Chimbuko la Ukoo = KAUKI

Chimbuko la Ukoo = KAUKI
KAUKI

UMOJA WA UKOO WA KIVENULE (KAUKI)

UMOJA WA UKOO WA KIVENULE (KAUKI)
TANGAZO LA MKUTANO MKUU WA 14 WA KAUKI

Jumatatu, 15 Aprili 2024

CHIMBUKO NA HISTORIA YA UKOO WA KIVENULE

 

Toleo la Kwanza - 2013


UKOO NI NINI?

Ukoo ni muungano wa familia kadhaa zenye utambulisho fulani. Unaweza kuwa utambulisho wa jina, alama au mwelekeo mmoja. Utambulisho wowote kati ya hizo nilizotaja, unaufanya ukoo utambulike miongoni mwa jamii mbalimbali. Mara nyingi utambulisho ambao huufanya ukoo utambulike baina ya jamii za Kiafrika ni Jina. Pamoja na jina, halikadhalika kuna tunu (values) mbalimbali ambazo huheshimiwa na ukoo husika na jamii kwa ujumla.

Tunu hubeba mambo mengi, ikiwa ni pamoja na miiko, maadili, heshima, vyakula na tamaduni. Sambamba na tunu, pia kuna Mila na Desturi, ambazo huzingatiwa sana katika masuala ya kijamii, mfano wakati wa kuoa au kuoza, misiba, sherehe za jadi mfano matambiko na masuala ya kimila.

Ukoo wa Kivenule ni mmojawapo wa koo nyingi kubwa zilizopo katika Himaya ya Uhehe katika Mkoa wa Iringa. Ukoo wa Kivenule ulianza kutambulika toka Karne ya 18. Historia inaonesha kuwa Ukoo huu asili yake ni kutoka kwa Wabena-Manga, waliopo Kusini mwa Mji wa Iringa; yaani maeneo ya Mufindi na Njombe. Ni mchanganyiko wa Wahehe na Wabena wanaojulikana kama Wabena-Manga.

Wahehe ni moja kati ya makabila makubwa hapa Tanzania ambalo kiasili linaishi katika Wilaya za Kaskazini mwa Mkoa wa Iringa, yaani Iringa Vijijini, Iringa Mjini, Kilolo na Mufindi. Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali zinazopatikana na kutafitiwa, inasemekana kuwa ni moja kati ya makabila yaliyotokea kwenye bonde la mto Rufiji; yaani Wahehe wenye Asili ya Ungazija. Pengine hata ile sababu ya kuzika wafu wao wakielekea mashariki inapewa uzito.

Lugha ya Kabila hili ni Kihehe na limegawanyika kiasi fulani katika lahaja (matamshi) tofauti tofauti kutokana na maeneo ambayo huzungumzwa. Inafanana kimatamshi na kimaana na lugha ya Kibena iliyopo wilayani Njombe. Pamoja na Wabena wanaohesabika kuwa zaidi ya watu milioni moja. Wengi wao ni wafuasi wa Ukristo, hasa wa Kanisa Katoliki (Jimbo Katoliki la Iringa). Kihistoria Wahehe ni maarufu kwa jinsi walivyopambana na Wajerumani walioteka maeneo yao, kama katika mapigano ya Lugalo mwaka 1891. Kiongozi wao alikuwa Chifu Mkwawa.

 

Katika kuenzi na kutunza tunu za asili za Uhehe, Ukoo wa Kivenule hauli nyama ya Mbawala (kwa lugha ya Kihehe Mato/Imato). Imani kubwa imejengeka miongoni mwa jamii ya Ukoo wa Kivenule kuwa kula Mbawala ni kuvunja miiko ya Ukoo ambayo iliyowekwa na Waasisi wetu (Babu zetu). Mara mwanaukoo anapokiuka miiko hii na kula nyuma ya Mbawala (Imato) basi huweza kufikwa na matatizo mbalimbali, mfano kudhurika afya yake. Mara nyingi huwapata matatizo kama ya kuvimba miguu na pengine kuoza kabisa.

 

Tunu nyingine ambazo Ukoo wa Kivenule unazienzi kama zilivyo koo nyingine katika Uhehe ni Miitikio (Midikiso). Tunu hii huutambulisha Ukoo wa Kivenule miongoni mwa Koo za Wahehe. Mwitikio (Mwidikiso) wa Ukoo wa Kivenule ni 'MLIGO'. Mwitikio huu hutumika katika maeneo mbalimbali mfano katika salamu, kuapa (kufanya viapo) na pia kujitofautisha na koo nyingine. Miitikio (Midikiso) huutambulisha Ukoo wa Kivenule katika koo nyingine katika ardhi ya Uhehe.

 

CHIMBUKO LA UKOO WA KIVENULE

Historia ya Chimbuko la Ukoo wa Kivenule limetoka mbali zaidi hata kabla ya Jina la sasa la KIVENULE kupatikana. Utafiti unaonesha kuwa BABU NYAKUDIRA BALAMA ndiye aliyemzaa (Baba yake) BABU KANOLO BALAMA. Hapa tunauangalia Ukoo wa Balama. Hali kadhalika, BABU KANOLO BALAMA, akamzaa BABU MTENGELINGOMA BALAMA. Maelezo haya yote tunayoyazungumzia ni katika Karne ya 17 kabla ya kuja kwa BABU TAGUMTWA BALAMA, ambaye aliuleta Jina la KIVENULE.

 

BABU MTENGELINGOMA BALAMA ndiye Baba Mzazi wa TAGUMTWA BALAMA. Wakati huu Babu Tagumtwa Balama alikuwa hajaenda kwenye Vita za LIGALU.

 

Kwa Asili, Ukoo wa Balama na baadaye Kivenule ni maarufu kama Wapiganaji wa Vita. Ukoo wa Balama (Kivenule) ulikuwa hodari sana katika vita vya msituni ambavyo viliwahusisha Babu zetu akina TAGUMTWA. Enzi hizo za Mababu zetu vita za Koo na Kabila zilipiganwa maeneo mengi ya himaya ya Uhehe kwa lengo la kupata mali, mifugo na heshima.

 

Babu TAGUMTWA BALAMA (KIVENULE) ndiye aliyewazaa Babu TAVIMYENDA KIVENULE na Babu KALASI KIVENULE. Ikumbukwe kuwa, jina halisi la ukoo wa Kivenule ni BALAMA. Kama ilivyokwisha julikana katika mada zilizowasilishwa katika Mikutano Mikuu Tisa ya Umoja wa Ukoo wa Kivenule (KAUKI), ambapo ilielezwa kuwa, neno KIVENULE linamaanisha sifa ya kuwa jasiri Vitani na hasa katika kutumia silaha za Mishale na Mikuki yaani kwa Lugha Asilia ya Kihehe “KUMIGOHA”.  Yaani kwa maana nyingine LIGALU yenye maana ya Kwihoma Imigoha – Kuhoma Vatavangu au Kuvenula AvatavanguLIGALU maana yake VitaKuhoma maana yake Kuchoma na Migoha maana yake MikukiVenula maana yake ua, fyeka maadui.

 

LIGALU ndiyo iliyochangia kuzaliwa kwa jina la Ukoo la KIVENULEKIVENULE maana yake ni Ushujaa kutokana na Shabaha ya Mikuki.

KUVENULA likiwa na maana halisi ya kuwa na shabaha ya kuwaangamiza maadui kwa kutumia silaha ya Mishale na Mikuki. Babu zetu akina TAGUMTWA BALAMA walilidhihirisha hili katika Vita na Watavangu na hivyo kusababisha kuzawadiwa kwa jina la KIVENULE kama jina la sifa kutokana na ushujaa katika Vita.

 

Tagumtwa Balama asili yake ni kutoka katika Ukoo wa Balama. Sifa kubwa ya Tabu Tagumtwa, alikuwa ana Shabaha sana ya Mikuki katika uwanja wa Vita. Alikuwa hakosei shabaha (target) na hivyo hupelekea kuwaangamiza na kuwaua sana maadui. Wakati akiwamaliza/fyeka/kuwaua adui zake kwa Mikuki, Wakuu wa Vita (Vatavangu) walikiita kitendo hicho 'KUVENULA'. Taarifa za Tagumtwa kuua (Kuvenula) adui zake katika uwanja wa vita, zilizagaa kila mahali na hivyo kupelekea Wakuu (Viongozi) wa Vita (Vatavangu) kumzawadia Jina la KIVENULEkama jina la sifa na heshima kwa kuwa shujaa wa Vita.

 

Ikumbukwa kuwa asili ya Ukoo wa Kivenule ni kutoka katika ukoo wa BALAMA (MWIBALAMA). Hawa ni ndugu wa karibu wa Kivenule kabisa na hawapaswi kuoana. Koo za Mwibalama zinapatikana maeneo mengi katika Mkoa wa Iringa hususani katika Wilaya  za Mufindi, Iringa Vijijini, Iringa Mjini na Kilolo; hali kadhalika kama ilivyo ukoo wa kina Mwakivenule.

 

TAGUMTWA KIVENULE alifia katika uwanja wa mapambano (vita) na mwili wake haukuweza kupatikana. Kama zilivyo koo za machifu au watu maarufu miili yao ilikuwa haizikwi. Baada ya kufa iliegemezwa kwenye miti mikubwa na kuliwa na wanyama. Wakija watu wasiukute mwili basi huamini kuwa mwili umechukuliwa na Mungu.

 

KUKUA NA KUZAGAA KWA UKOO WA KIVENULE

Kwa mujibu wa taarifa mbalimblai za kitafiti ambazo zimekuwa zikifanyika toka mwaka 2005 hadi sasa 2013; kupitia mikutano mbalimbali ya KAUKI; zinabainisha kuwa, BABU         NYAKUDIRA BALAMA  alimzaa BABU KANOLO BALAMA. Hali kadhalika BABU KANOLO BALAMA alimzaa MTENGELINGOMA BALAMA. BABU MTENGELINGOMA BALAMA ndiye aliyemzaa Tagumtwa Balama (Kivenule).

 

Baada ya hapo, tunaona sasa Kizazi cha TAGUMTWA KIVENULE kinaanza kujitokeza. Hii ilikuwa ni Karne ya 18. TAGUMTWA KIVENULE alizaa watoto wawili (2).  Bado utafiti unafanyika kumfahamu Mama wa watoto hawa. Watoto wa Tagumtwa Kivenule walikuwa ni TAVIMYENDA KIVENULE na KALASI KIVENULE. Kwa mujibu wa taarifa kadhaa tulizonazo kwa sasa; hawa ni vinara wa Ukoo wa Kivenule ulioenea maeneo mbalimbali hapa Tanzania.

 

Tavimyenda Kivenule na Kalasi Kivenule katika harakati za kutafuta maisha walifika katika eneo la Kalenga, mahali alipoishi Mkwawa na kukutana na na Mwamyinga, aliyekuwa mfugaji maarufu katika eneo la Ulefi huko Magubike, Iringa Vijijini. Tavimyenda Kivenule alibahatika kupata kazi kwa Mwa-Myinga baada ya kuombwa kwenda kumwangalizia mifugo yake huko Magubike, huku akimwacha mwenzake Kalasi pale Kalenga.

 

Kalasi Kivenule yeye hakupata fursa hiyo ya kazi na hivyo akaamua kuelekea eneo Irore katika Wilaya Iringa Vijijini (kwa sasa Kilolo) kutafuta maisha. Huu ukawa ni mwanzo wa kugawanyika kwa watoto hawa wawili wa Tagumtwa Kivenule.

 

Tavimyenda Kivenule akielekea upande wa Magharibi mwa Mji wa Iringa na Kalasi alielekea upande wa Mashariki mwa Mji wa Iringa.

 

Historia inabainisha kuwa pamoja na Babu hawa kugawanyika kutokana na utafutaji wa maisha, mahusiano na ushirikiano baina yao haukuvunjika. Babu zetu waliendelea kushirikiana na kutembelea licha ya ukoo kukua na kuwa mkubwa sana.

 

KIZAZI CHA TAVIMYENDA KIVENULE

Katika Karne ya 19 hadi 20, Kizazi cha Tavimyenda Kivenule kilizaliwa na kuzagaa katika maeneo ya Ulefi, Magubike na Mlafu, Wilaya ya Iringa Vijijini, Iringa Mjini na maeneo mengine mkoani Iringa.

 

Taarifa tulizonazo kupitia tafiti tunazofanya, hali inaonesha kuwa, Babu Tavimyenda alikuwa na wake watatu (3), ambao ni:

1.    Bibi       Mkami       Sekabogo

2.    Bibi       Senosa

3.    Bibi       Pili            Mvemba

 

Mke wa kwanza wa Tavimyenda Kivenule aliolewa akiwa na mtoto; aliyejulikana kama Bibi Sikimbilavi Semabiki. Kwa mke huyu wa Kwanza Sekabogo, Tavimyenda alizaa nae watoto wanne (4); ambao ni:

1.    Babu     Kavilimembe      Kivenule

2.    Babu     Mgaifaida           Kivenule

3.    Babu     Sigatambule               Kivenule

4.    Babu     Hussein             Kivenule (Bado yupo hai)

 

Kwa Mke wa Pili Bibi Senosa, Babu Tavimyenda akizaa nae watoto watatu (3); ambao ni:

1.    Babu     Abdallah            Kivenule

2.    Bibi       Sigungilimembe  Kivenule

3.    Bibi       Malibora            Kivenule

Watoto hawa wa Bibi Senosa waliishi maeneo ya Kihesa katika Mji wa Iringa.

 

Kwa upande wa mke wa Tatu wa Bibi Pili Mvemba; Babu Tavimyenda alizaa mtoto mmoja aliyejulikana kwa jina la BIBI MGASI KIVENULE aliishi eneo la Ulefi. Baada ya kufariki amezikwa Mlafu. Babu Tavimyenda Kivenule amezikwa katika eneo la Ulefi.

 

Bibi SIKIMBILAVI alikuwa mtoto wa kufikia wa Bibi MKAMI SEKABOGO. Bibi SIKIMBILAVI aliolewa na Ukoo wa Mgoda na kubahatika kupata watoto wanne (4) ambao ni:

1.    Mama wa Kitatambe

2.    Salia     Maneno     Mgoda

3.    Galamale Mgoda

4.    William Mgoda

 

Baada ya hapo kizazi hiki kimeendelea kukua hadi hivi sasa Karne ya 21. **Angalia Chati kuonesha Muundo wa Ukoo wa KIVENULE**

 

KIZAZI CHA KALASI KIVENULE

Kwa upande wa Kalasi Tagumtwa Kivenule, kizazi hiki kilienea maeneo ya Nduli, Mgongo, Itagutwa, Kigonzile, Igominyi na Irore. Taarifa zinaonesha kuwa, Babu Kalsi Kivenule alikuwa na wake wawili (2); yaani:

1.    Bibi       Semsakwa                 Mnonikilwa

2.    Bibi       Mnyamtage                Sekindole

 

Bibi Semsakwa Mnoni Kirwa kwa Babu Kalasi Kivenule alizaa watoto wawili (2) ambao ni:

1.    Bibi Cheilaje Nginasambula Kivenule

2.    Gingilemesa Kivenule

 

Kwa bahati mbaya hakuna taarifa zozote za hawa watoto wawili wa Kalasi.

 

Kwa upande wa Bibi Mnyamtage Sekindole, Babu Kalasi Kivenule alizaa mtoto mmoja ambaye ni Salamalenga Kahengula Kivenule. Bibi Mnyatage Sekindole awali alikuwa ameolewa kwa Mwa-Mhumba na kuzaa nae mtoto mmoja aliyeitwa Bibi Mganga Semhumba na baadaye kufariki. Baada ya hapo aliolewa na Kalasi ambapo pia alizaa mtoto mmoja tu anayefahamika kwa jina la Salamalenga Kahengula Kivenule. * Angalia watoto wa Kahengula katika Chati ya Muundo wa Ukoo wa Kivenule*

 

Kuna taarifa nyingi kutoka kwa Babu Tavimyenda Kivenule na Kalasi Kivenule. Mwingiliano wa koo nao unaonesha simulizi hizi. Kwa upande wa Tavimyenda mke wa Kwanza Bibi Mkami Sekabogo alikuwa na mtoto wa kufikia, aliyejulikana kwa jina la Bi Sikimbilavi Semabiki. Hatujapata taarifa rasmi kuhusiana na kizazi cha Bibi huyu, kama ilivyotokea kuwa Sipanganakumtwa Mwilongo Regina Sematagi aliyekuwa mtoto wa kufikia Bibi Semkonda mke wa Salamalenga Kahengula Kivenule.

 

Sipanganakumtwa Mwilongo Regiona Sematagi amesaidia kueneza kizazi cha Ukoo wa Mnyavanu. Taarifa zaidi na ukoo wa Mnyavanu upo katika Chati ya Chimbuko na Muundo wa Ukoo wa Kivenule.**

 

TABIA YA KIZAZI CHA TAVIMYENDA NA KALASI KIVENULE KUOA WAKE WENGI

Tabia nyingine ya kizazi hiki cha Tavimyenda na Kalasi ilikuwa ni kuoa wake wengi. Kwa mfano Tavimyenda pekee alikuwa na wake watatu. Hali kadhalika Kalasi naye alikuwa na wake wawili.

 

Hali hii ya kuwa na mke zaidi ya mmoja walirithi watoto wao. Kwa mfano watoto watatu wa kiume wa Tavimyenda waliozaliwa kwa Bibi Mkami Sekabogo walioa wake wawili hadi watatu. Mtoto wa kwanza wa Babu Tavimyenda Kivenule aliyejulikana kama Kavilimembe Kivenule alikuwa na wake wawili (2). Mtoto wa tatu wa Bibi Mkamai Sekabogo, aliyejulikana kwa jina la Sigatambule Matesa Kivenule, alikwa na wake watatu. Hali kadhalika mtoto wa nne wa Bibi Mkami Sekabogo anayejulikana kama Hussein Kivenule alikuwa na wake wawili. Mtoto pekee wa Pili wa Bibi Mkami hakubahatika kuwa na familia; na alijiita jina la kujinyanyapaa "Mgaifaida" Kivenule.

 

Sambamba na tabia ya Ukomo wa Kivenule kuoa mke zaidi ya moja; pia kuna utamaduni uliojitokeza kwa baadhi ya watoto wa Bibi Mkami Sekabogo kuoa dada na mdogo wake. Hili linajidhihirisha kwa wake wawili wa Babu Kavilimembe Kivenule ambao walikuwa ni Bibi Sikumwendinguluvi Sekusiga (Bi Mkubwa) na Bibi Gakumwalia Sekusiga (Bi Mdogo).

 

Hali kadhalika kwa mtoto wa tatu wa Bibi Mkami Sekabogo; Babu Sigatambule Matesa Kivenule alioa wake watatu, ambapo wake wawili wakubwa, 'Bibi Sikumwendinguluvi Singaile (Bi Mkubwa) na Bibi Nyanyilemale Singaile (Bi Mdogo wa Pili); na wa tatu aliitwa Bibi Pangulimale Setwanga.

 

Mtoto wa nne wa Bibi Mkami Sekabogo Hussein Kivenule, yeye alioa wake wawili kutoka familia tofauti. Wake zake waliitwa Bibi Yimilengeresa Semsisi (Bi Mkubwa) na Bibi Dalika Setala (Bi Mdogo). Kwa upande wa watoto Kalasi Kivenule, mtoto wake Salamalenga Kahengula Kivenule naye alioa wake watatu; ambao ni Bibi Semkonda, Bibi Semfilinge na Bibi Nyangali.

 

Hatujapata taarifa rasmi za watoto wa Kalasi kutoka kwa mke wake Bibi Semsakwa Mnonikilwa ambao ni Cheilaje Nginasambula Kivenule na Gingilemesa Kivenule. Kwa upande wa Kahengula yeye alioa kutoka katika familia tofauti.

 

 

UZAO WA BABU KAVILIMEMBE, MGAIFAIDA, SIGATAMBULE NA HUSSEIN KIVENULE

Babu Kavilimembe Kivenule aliishi eneo la Magubike, Wilaya ya Iringa Vijijini, huku akipakana na Ulefi upande wa Kaskazini, Idete na Ibogo upande wa Magharibi. Akiwa ameoa wake wawili wa familia moja, Babu Kavilimembe alibahatika kupata watoto sita (6).

 

Kwa upande wa mke wa kwanza Bibi Sikumwendinguluvi Sekusiga; Mzee Kavilimembe Kivenule alipata watoto wafuatao:

1.    Elizabert                Kivenule

2.    Dalikimale      Kivenule

3.    Sandra          Kivenule

4.    Pangalasi       Kivenule

 

Na kwa mke mdogo Bibi Gakumwalia Sekusiga, Mzee Kavilimembe alipata watoto wawili ambao ni:

1.    Salikuvaganga        Kivenule

2.    Francis         Kivenule

 

Watoto hao wa Babu Kavilimembe wengi wao waliishi maeneo ya Ulefu na Magubike. Baadhi yao walihamia maeneo mengine kama Nzihi, ukiacha wale waliokuwa watumishi wa serikali wakaenda kuishi maeneo mbalimbali. Babu Kavilimembe amezikwa eneo la Magubike, Iringa Vijijini.

 

Kwa upande wa Babu Mgaifaida (Yakobo) Kivenule, yeye hakubahatika kupata familia. Mgaifaida alikuwa na ulemavu ambao ulimfanya ashindwe kutembea katika hali ya kawaida. Muda mwingi aliishi eneo la Ulefu kabla ya sehemu kubwa ya Ukoo wa Kivenule kuhamia sehemu ya Mlafu. Baada ya kufariki, alizikwa Mlafu.

 

Babu Sigatambule Matesa Kivenule alikuwa ni mtoto wa tatu wa Tavimyenda Kivenule kwa Bibi Mkami Sekabogo. Babu Sigatambule aliishi Ulefi, akahamia Mlafu na baadaye Kidamali. Babu Sigatambule ndiye aliyehakikisha Ukoo wa Kivenule unapata eneo la Mlafu huku akipambana na Wagiriki. Walowezi na wawekezaji katika zao la Tumbaku.

 

Babu Sigatambule Kivenule katika uhai wake alibahatika kuoa wake watatu (3); huku wake zake wawili wakitoka katika familia moja ya ukoo wa Singaile. Wake zake hawa wakubwa waliitwa Bibi Sivangumhavi Singaile na Bibi Nyanyilimale Singaile. Mke wa Tatu wa Babu Sigatambule aliitwa Bibi Pangulimale Setwanga. Wote waliishi Mlafu na baadaye kuhamia eneo Kidamali.

 

Wake zake wawili Bibi Nyanyilimale Singaile na Bibi Pangulimale Setwanga bado wapo hai na wanaishi Kidamali mpaka leo.

 

Watoto wa Babu Sigatambule Kivenule ni hawa wafuatao:

Kwa Bibi Sivangumhavi Singaile (Mke Mkubwa):

1.    Gidagumhindi         Cecilia       Kivenule

2.    Semyamba    Khadija      Kivenule

3.    Sivinitu          Alphonce   Kivenule

4.    Kadungu                William      Kivenule

5.    Fibumo          Xavery      Kivenule

6.    Mlagile          Anyesi       Kivenule

7.    John                             Kivenule

 

Bibi Nyanyilimale Singaile (Mke wa Pili)

1.    Mgulwa         Agnes        Kivenule

2.    Luhanage      Ponsiano    Kivenule

3.    Mgendwa       Eusebio     Kivenule

4.    Msinziwa                Daniel       Kivenule

5.    Kanolo          Edward      Kivenule

 

Mke wa Tatu wa Bibi Pangulimale Setwanga

1.    Conjeta         Kivenule

2.    Pyela    Kivenule

3.    Faustino Kivenule

4.    George  Kivenule

5.    Carolina Kivenule

 

Babu Sigatambule Kivenule alifariki mwaka 1995 na kuzikwa eneo la Mlafu, Kidamali - Iringa. Hali kadhalika mke wake Mkubwa Bibi Siwangumhavi Singaile Mwilumbwa alifariki dunia mwaka 1999 na kuzikwa eneo hilo hilo la Mlafu.

 

Mzee Hussein Tavimyenda Kivenule alikuwa ni mtoto wa nne wa Bibi Mkami Sekabogo. Yeye aliishi eneo la Ulefi na baadaye Mlafu. Hatimaye alihamia Magubike. Babu Hussein Kivenule hadi anafariki dunia Juni 26, 2013 anakadiriwa kuwa na miaka zaidi ya 113 kwa mujibu wa taarifa na tafiti ambazo tunazo.

 

Babu Hussein Tavimyenda Kivenule ameshiriki kikamilifu katika Vita vya Pili ya Dunia. Wakati anashiriki vita hiyo alikuwa na umri wa zaidi ya miaka 44. Amepigana vita maeneo mbalimbali mfano Burma, India na Ulaya. Kwa sasa ana upofu wa macho ambao anasema ulisababishwa na Baruti. Hali kadhalika anakiri kuwa kuendelea kuwa hai ni kwa sababu alipigana upande wa Mwingereza. Anakiri vita ndiyo iliyomsababishia upofu pengine asingekuwa na hali aliyonayo kwa sasa.

 

Mzee Hussein Kivenule alioa wake wawili na kubahatika kupata watoto kumi na tatu (13). Kwa mke wake wa kwanza Bibi Yimilengeresa Semsisi. Babu Hussein alipata watoto wafuatao:

1.    Nyakudila      Benjamin   Kivenule

2.    Sekiyavile      Modesta    Kivenule

3.    Dominicus                     Kivenule

4.    Emmanuel                     Kivenule

5.    Luciana                         Kivenule

6.    Ajendina                        Kivenule

 

Kwa upande wa mke wa pili wa Bibi Dalika Setala, Mzee Hussein Kivenule alipata watoto wafuatao:

1.    Kabogo Bernadi      Kivenule

2.    Sembata Josephine         Kivenule

3.    Necia                    Kivenule

4.    Batromeo              Kivenule

5.    Brandino             Kivenule

6.    Tavina                  Kivenule

7.    Masikitiko              Kivenule

 

Asilimia kubwa ya familia ya Babu Hussein Kivenule inaishi maeneo ya Magubike, Idete na Ibogo. Pia wapenda historia mnakaribishwa kwenda kumtembelea Babu Hussein Kivenule.

 

UZAO WA SALAMALENGA KAHENGULA KIVENULE

Babu Salamalenga Kahengula Kivenule alikuwa ni mtoto pekee wa kiume wa Babu Kalasi kwa mke wake wa pili Bibi Mnyamtage Sekindole. Kahengula pia ni kaka wa Bibi Mganga Semhumba, aliyekuwa mtoto pekee kwa Mwamhumba, aliyefariki mara tu baada ya kumzaa Bibi Mganga kwa Sekindole.

 

Babu Salamalenga Kahengula Kivenule alio wake watatu ambao ni:

1.    Bibi Semkonda

2.    Bibi Semfilinge

3.    Bibi Nyangali

 

Salamalenga anapomuoa Bibi Semkonda alimkuta na mtoto wa kufikia Sipanganakumtwa Mwilongo Regina Sematagi. Kwa wake zake hawa watatu, Babu Salamalenga alibahatika kupata watoto kumi na tatu (13). Kwa Bibi Semkonda alibahatika kupata watoto wafuatao:

1.    Pangayena     Kivenule

2.    Jonas            Kivenule

3.    Samwel                 Kivenule

4.    Galasamaneno       Kivenule

5.    Daud (William)       Kivenule

6.    Barton           Kivenule

 

Kwa mke wa pili Bibi Semfilinge, Babu Salamalenga alizaa nae watoto watatu ambao ni:

1.    Chogavanu            Kivenule

2.    Munguatosa           Kivenule

3.    Mwilimilisa             Kivenule

 

Na kwa mke wa tatu Bibi Nyangali, Babu Salamalenga alizaa nae watoto wanne (4) ambao ni:

1.    Tindasulanga          Kivenule

2.    Sigongola              Kivenule

3.    Shaban                 Kivenule

4.    Gungamesa           Kivenule

 

MWINGILIANO NA KOO NYINGINE KATIKA HIMAYA YA UHEHE

Zaidi ya Koo mbalimbali 50 zinachangamana na Ukoo wa Kivenule. Hii ni kutoka Karne ya 18 ambapo kizazi hiki kilianza kujitambua na kujikusanya. Baadhi ya Koo ambazo zimechangamana na ukoo huu ni pamoja na koo za:


1.    Kabogo

2.    Kamtawa

3.    Katowo

4.    Kigereso

5.    Kindole

6.    Kisumbe

7.    Kiteve

8.    Kitu

9.    Kusiga

10.           Lawa

11.           Luhwavi

12.           Lupola

13.           Madembwe

14.           Manimu

15.           Matagi

16.           Mdongwe

17.           Mfilinge

18.           Mhapa

19.           Mhumba

20.           Mkeng'e

21.           Mkonda

22.           Mnonikirwa

23.           Mnyavanu

24.           Msisi

25.           Mtono

26.           Mvemba

27.           Myalla

28.           Ngeng'ena

29.           Ngolo

30.           Ngwenga

31.           Ngweta

32.           Nyakunga

33.           Nyangali

34.           Nyangalima

35.           Twanga

36.           Nzala

37.           Sambagi

38.           Senosa

39.           Setala

40.           Singaile

41.           Utenga

42.           Kalinga

43.           Sungu

44.           Mgimwa

45.           Nyamika

46.           Nongele


 

Kwa taarifa na mawasiliano na:

Umoja wa Ukoo wa Kivenule (KAUKI)

http://www.tagumtwa-kivenule.blogspot.com

 

Chimbuko na Historia ya Ukoo wa Kivenule

http://kauki-kauki.blogspot.com/2013/08/chimbuko-na-historia-ya-ukoo-wa-kivenule.html 

Jumapili, 14 Aprili 2024

KAMATI ZA MAANDALIZI YA MKUTANO MKUU WA 13 WA KAUKI


 

UONGOZI WA UMOJA WA UKOO WA KIVENULE (KAUKI) WAWAKUMBUSHA WANAUKOO KUHUSU MKUTANO MKUU


Viongozi wa Umoja wa Ukoo wa Kivenule (KAUKI) kwa niaba ya Wanaukoo Wote; wanayofuraha kubwa kuwakumbusha kuwa Mkutano Mkuu wa 13 wa KAUKI unatarajia kufanyika Siku ya Jumamosi ya tarehe 29 Juni 2024, Kijijini Kidamali, Mkoa wa Iringa. Mkutano huu ni Mwendelezo wa Mikutano ya Ukoo ambayo hufanyika kila Mwaka.

Ili kufanikisha Mkutano huo, Wanaukoo Wote wanaombwa kutoa Michango yao ili kufanikisha Mkutano huo. Watu Wazima Watachangia Shilingi 10,000/- na Watoto 5,000/-. Michango hii itasaidia upatikanaji wa huduma za Chakula, Chai na Maji kwa Siku zote tutakazokuwa Kidamali. Michango itolewe kwa Viongozi wa Kanda Husika.

 Malengo ya Mkutano Mkuu ni pamoja na:

1.     Kutambulishana na Kufahamiana Ndugu/Wanaukoo;

2.     Kujua Chimbuko na Historia ya Ukoo wa Kivenule;

3.     Kubadilishana Taarifa na Uzoefu Mbalimbali wa Shughuli za Maisha;

4.     Kuweka mikakati mbalimbali ya kuimarisha undugu na ushirikiano baina ya Wanaukoo; na mengineyo.

Mikutano ya KAUKI huhudhuriwa na Wanaukoo kutoka Maeneo ya Magubike, Kidamali, Kalenga, Nzihi, Nyamihuu, Nyamahana, Nduli, Mgongo, Itagutwa, Igominyi, Vilalo, Migoli, Iringa Mjini, Mafinga, Dar es Salaam, Morogoro, Mwanza na Maeneo mengine ambayo washiriki wanaishi.

 Imeandaliwa na Kutolewa na:


Uongozi wa KAUKI

 

Sambaza kwa Ndugu Wote.

MKUTANO MKUU WA 13 WA UMOJA WA UKOO WA KIVENULE (KAUKI)