
HISTORIA YA KAUKI
Umoja wa Ukoo wa Kivenule (KAUKI) ni sehemu ya harakati za Maendeleo zinazofanywa katika kujikwamua na kuondokana na matatizo mbalimbali yanayoikabili jamii hii. KAUKI hufanya mikutano kwa wanaukoo kama sehemu wa mwendelezo wa jitihada za namna hii ambayo imekuwa ikifanywa mara moja kila mwaka. Kwa mara kwanza katika historia, Mkutano Mkuu wa Kwanza wa Umoja wa Ukoo wa Kivenule, ulifanyika, tarehe 17 – 18 Desemba 2005, katika Ukumbi wa Sanga, Kijijini Kidamali, mkoani Iringa. Umoja wa Ukoo wa Kivenule ulizinduliwa rasmi mwaka 2006, katika Mkutano Mkuu wa Pili wa Ukoo wa Kivenule uliofanyika tarehe 24 – 25 Juni 2006 katika Ukumbi wa Sanga Kijijini Kidamali, Iringa. Kuzinduliwa kwa Umoja wa Ukoo wa Kivenule, kulienda sambamba na uzinduzi wa Mfuko wa Ukoo pamoja na Kuipitisha Rasimu ya Katiba ya Umoja wa Ukoo wa Kivenule na hivyo kuwa Katiba Rasmi. Kuwepo kwa Katiba ya KAUKI kulitoa fursa ya kuanza kwa utekelezaji wa shughuli na mipango mbalimbali ya maendeleo. Pia, pamoja na mambo mengine, katika Mkutano Mkuu wa Pili wa Ukoo, kulifanya uchaguzi wa Viongozi wa Kanda, uchaguzi wa Walezi wa Ukoo na hivyo utendaji rasmi wa KAUKI kuruhusiwa kuanza.
Katika Mkutano Mkuu wa Kwanza wa Umoja wa Ukoo wa Kivenule (KAUKI), jumla ya ndugu/wanaukoo wapatao 129 toka sehemu mbalimbali mkoani Iringa na kwingineko hapa Tanzania waliohudhuria. Mkutano Mkuu wa Pili wa KAUKI ulihudhuriwa na jumla ya ndugu/wanaukoo wapatao 140. Baadhi ya ndugu/wanaukoo waliohudhuria mikutano hiyo walitoka sehemu za Kidamali, Nyamihuu, Ilala-Simba, Nyamahana, Magubike, Kipera, Nduli, Iringa Mjini, Morogoro, Mikumi, Dar es Salaam, Mufindi, Mbeya, Kilimanjaro, Tosamaganga, Mseke, Mwanga, Kalenga, Idodi, Mgongo, Ilole, Itagutwa, Kipera, Idete na Nzihi.
Mkutano mkuu wa tatu wa KAUKI umezidi kupanua wigo, maono na mipango inayohusiana na maendeleo ya umoja huu. Mahudhurio ya washiriki katika mkutano pia nayo yamepanuka kutokana na kupata washiriki wapya wengi zaidi kutoka maeneo ya Ilole, Nduli, Mgongo na Mufindi.
Japo safari hii, mahudhurio ya wanaukoo nje ya mkoa wa Iringa hayakuwa ya kuridhisha katika ilivyofanyika katika MKutano Mkuu wa Pili wa KAUKI – 2006. Kwa mfano hapakuwepo na mwakilishi yeyote toka katika mkoa wa Kilimanjaro kama ilivyokuwa mwaka 2006. Mahudhurio toka mkoa wa Dar es Salaam yalikuwa nia madogo sana ilinganishwa na mwaka 2006.
Kwa wastani uwakilishi wa ndugu/wanaukoo waliohudhuria Mkutano Mkuu wa Tatu wa Ukoo wa Kivenule haukuwa wa mtawanyiko zaidi katika ilivyojidhihirisha katika mkutano mkuu wa pili wa KAUKI. Hii kwa Umoja wa Ukoo wa Kivenule ni changamoto kubwa ambayo inabidi ifanyiwe kazi.
Japo baadhi ya malengo ya umoja huu yalianza kujidhirisha katika mkutano mkuu wa pili wa KAUKI, hali ni tofauti kabisa katika mkutano mkuu wa tatu. Tofauti baina ya ndugu/wanaukoo zimeendelea kujidhihirisha. Hii imechangia pia mahudhurio kuwa duni hususani kwa wanaukoo toka eneo la Kidamali. Suala jingine ambalo limechangia mahudhurio duni ni uchangaji wa michango ya kufanikisha Mkutano Mkuu wa Tatu wa KAUKI. Kamati ya Maandalizi ya Mkutano Mkuu wa Tatu toka Kidamali ilipitisha uamuzi wa kutowaalika ndugu/wanaukoo ambao hawakuonyesha nia ya kuchangia au kuchangia kabisa.
Kwa KAUKI haya siyo malengo yake, lakini kuna wakati inabidi kukubaliana na hali halisi ili kuweza kukamilisha baadhi ya shughuli ambazo zinakuwa zimepangwa kufanyika. Baada ya kufanya tathmini, uongozi wa KAUKI ulikubaliana na uamuzi wa Kamati ya Maandalizi ya Kidamali ya kuwazuia kuhudhuria mkutano mkuu wa tatu wa KAUKI wale ndugu/wanaukoo ambao hawakuchangia chochote ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Kutokana na ufinyu wa bajeti na pia kukosa vyanzo vingine vya mapato, inabidi taratibu nyingine ambazo ni kinyume cha malengo ya KAUKI kuruhusiwa kutumika ili kunusuru baadhi ya shughuli zinazokusudiwa kufanyika. Japo KAUKI haikuridhishwa na uamuzi wa kuwazuia baadhi ya ndugu/wanaukoo ambao hawakuchanga michango kwa ajili ya maandalizi ya mkutano, haikuwa na namna nyingine ya kuweza kusaidia tatizo hilo kutokana na kukosa fedha toka katika mfuko wake.
Jambo la kufurahisha zaidi ni kupanuka kwa wigo wa mahudhurio na mwitikio katika mikutano hii; na pia kuanza kutolewa kwa fursa ya kufanya mikutano ya namna hii sehemu nyingine mfano Mkutano Mkuu wa Nne wa KAUKI utafanyika Ilole. KAUKI inaamini hii fursa nzuri ya jamii husika kutoka katika maeneo ambako mkutano unafanyika kuhamasishana wenyewe kwa wenyewe na hivyo kuongeza ari na moyo wa ushirikiano.
Viongozi wa Umoja wa Ukoo wa Kivenule bado wanaamini kuwa hawajatimiza lengo lao la kuandaa mikutano ya namna hii kwa kiwango cha juu; kwani wanaamini kuwa bado kuna idadi kubwa ya ndugu/wanaukoo ambao bado hawajapata fursa ya kuhudhuria mikutano hii. Ndiyo maana, Umoja wa Ukoo wa Kivenule bado unahamasisha ndugu/wanaukoo wahamasishane kuhudhuria mikutano hii.
Vijiji ambavyo vimeonyesha mwelekeo mzuri na ambapo kwa Viongozi wa Ukoo ni mafanikio makubwa ni pamoja na Kidamali, Nyamihuu, Ilala-Simba, Nyamahana, Magubike, Idete na Nzihi. Pia, maeneo ya Nduli, Ilole na Mgongo, zimeonyesha mwelekeo mzuri na ndiyo maana Mkutano Mkuu wa Nne wa KAUKI unafanyika Ilole ikiwa ni mzunguko uliopangwa kuanza kutekelezwa baada ya mikutano mitatu (3) ya KAUKI kufanyika Kidamali. Umoja wa Ukoo wa Kivenule unadhani kuwa hii changamoto tosha kwa viongozi pamoja na ndugu/wanaukoo toka sehemu husika kudhihirisha ari yao na jinsi wanavyohamasika kuutumia umoja huu wa KAUKI kuunganisha ukoo na nguvu zao.
Kuendelea kufanyika kwa mikutano ya KAUKI ni sehemu ya mapambano na pia harakati endelevu za kukabiliana na mabadiliko ya kisera, kisiasa, kiuchumi, kijamii, kiutamaduni, kisayansi na teknolojia, na hususani utandawazi na soko huria ambayo yanapelekea jamii kubwa ya Watanzania kuwa tegemezi. Kwa kutambulia hilo, KAUKI inajaribu kutafuta mbadala/mwafaka wa changamoto hizi kwa kuunganisha nguvu ya wanajamii wanaounda KAUKI kushiriki kikamilifu katika masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo hasa suala la kupata elimu, kuwa na hali nzuri kiuchumi na kimaisha na kuyakubali mabadiliko ya dunia na hivyo kuchukua hatua mahsusi kuweza kukabiliana nayo.
UKIMWI, ufisadi, njaa, umaskini uliopindukia ni sehemu ya matatizo na changamoto kubwa zinayoikabili KAUKI. Mabadiliko ya hali ya hewa, uharibifu wa mazingira ni changamoto ambayo Ukoo wa Kivenule unawajibu wa kukabiliana nayo. Athari na
madhara ya majanga hatarishi tayari yanaonekana katika jamii zetu na katika maisha yetu ya kila siku. Mfano ongezeko la watoto yatima, watoto wa mitaani wasio na walezi, kuongezeka kwa utegemezi kutokana na wajane kutokuwa na msaada baada ya kupoteza/kufiwa na ndugu/wanaume zao kutokana na maradhi ya UKIMWI bado ni tatizo kubwa.
Jamii hii tegemezi tunayoijenga na ambayo tunaishuhudia ikikua pole pole siku hadi siku, inatutegemea sisi ndugu/wanaukoo wa kila kitu. Kwa mfano jamii yetu ina wajibu wa kuhudumiwa chakula, malazi, mavazi, madawa, nyumba nzuri za kuishi na elimu. Je, jamii hii itaweza kukabiliana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia kama sisi kama wanajamii husika tutashindwa kukubali kuwajibika kwa kuwapa elimu na huduma zingine za msingi? Hii ni changamoto kubwa ambayo hatuna budi kuifanyia kazi, na kila ndugu/mwanaukoo kukubali kila jukumu ambalo atakuwa amepewa na jamii inayomzunguka.
Nasi kama jamii inayounda Ukoo wa Kivenule tuna wajibu wa kushirikiana na asasi za kijamii na kiserikali katika kuleta maendeleo. Wimbi la umaskini uliokithiri, janga la UKIMWI, ujinga na rushwa vimekuwa ni vikwazo vikubwa vya maendeleo na ambavyo vinazidi kudidimiza harakati mbalimbali za kuweza kujiinua na kujikwamua katika hali hiyo. Harakati hizi za kutafuta maendeleo zimegawanyika katika makundi mbalimbali ya kijamii hususani makundi ya wasomi, wakulima, wafugaji, wafanyabiashara, wanawake na wananchi wa kawaida.
Pia haja ya kufahamiana baina ya wanajamii na ndugu wanaounda ukoo, pamoja na kuujua Ukoo kwa ujumla ni sehemu ndogo tu ya changamoto japo ina madhara makubwa zaidi kama wanaukoo hawafahamu. Kuwa wengi ni sehemu ya raslimali. Kama tunahitaji maendeleo, tunahitaji watu, uongozi bora na siasa safi. Japo suala la fedha ni muhimu, lakini kama huna mipango thabiti, fedha inaweza isiwe muhimu kwani itapotea bure bila kufanya jambo la msingi.
Kuna baadhi ya majukumu muhimu bado hayajafanyiwa kazi. Mfano sensa haijafanyika ili kuweza kujua idadi ya ndugu/wanaukoo wanaounda KAUKI. Bila kujitambua sisi wenyewe hatuwezi kutekeleza mipango yetu kama wana-KAUKI. Sensa ni muhimu sana kwa kuandaa mipango yetu na pia kujiwekea malengo yetu kama wana-KAUKI.
Changamoto zitakazopatikana baada ya kuyagusia mambo haya ya msingi katika mikutano hii inayofanyika, pia inawapa fursa washiriki wa mikutano hiyo kujenga ajenda mpya za mikutano ijayo.
Mkutano mkuu wa kwanza wa KAUKI uliyaangalia kwa kina mahusiano duni baina ya wana ndugu, kukosekana kwa ushirikiano katika mambo mbalimbali ya kimaendeleo, hali duni ya kiuchumi na kijamii, matatizo ya kifamilia na kiukoo.
Mwelekeo na nafasi ya ukoo wa Kivenule katika suala nzima la Elimu hasa katika dunia hii ya Utandawazi (Globalization). Maendeleo ya sayansi na teknolojia ambapo yameifanya dunia kuwa kama kijiji kisicho na mipaka na kila mtu anaruhusiwa kuingia na kutoka; kuongezeka kwa viwanda vinavyotumia teknolojia ya hali ya juu; kuongezeka kwa teknolojia ya habari na mawasiliano (Internet); kupanuka na kujengeka kwa miji, pamoja na soko huria. Mambo yote haya ndiyo yanayoweza kuonyesha mustakabali na nafasi ya ukoo wa Kivenule kwa maisha ya baadaye. Bado inajidhihirisha kuwa ukoo wetu upo nyuma sana katika suala nzima la elimu, hii linajidhihirisha kutokana na kuwa na ndugu wachache sana ambao wameweza kupata elimu kwa kiwango kinachostahili. KAUKI inakabiliwa na changamoto za mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia yanayojitokeza kila kukicha na yanayoibadili dunia na hivyo kutulazimisha nasi katika ukoo wa Kivenule kubadilika. Matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano katika simu za mikononi, Internet, kompyuta, redio na satelaiti ni changamoto kubwa katika Ukoo wa Kivenule.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni