Chimbuko la Ukoo = KAUKI

Chimbuko la Ukoo = KAUKI
KAUKI

UMOJA WA UKOO WA KIVENULE (KAUKI)

UMOJA WA UKOO WA KIVENULE (KAUKI)
TANGAZO LA MKUTANO MKUU WA 14 WA KAUKI

Jumapili, 30 Juni 2024

MKUTANO MKUU WA 13 WA KAUKI WAFANYIKA KIDAMALI - IRINGA

Umoja wa Ukoo wa Kivenule (KAUKI) umefanya Mkutano Mkuu wa 13 katika Kijiji cha Kidamali Mkoani Iringa. Mkutano huo umefanyika mnamo tarehe 29 – 30 Juni 2024, huku ukihudhuriwa na ndugu na wanaukoo zaidi ya 70 wakiwa na Vitambulisho vyao.

Mkutano Mkuu wa 13 wa KAUKI unafanyika kwa mara nyingine baada ya Mkutano Mkuu wa Mwisho wa Ukoo wa Kivenule uliofanyika katika Kijiji cha Vilalo, Irore Mkoani Iringa.

Baadhi ya Wanaukoo wa Kivenule waliohudhuria Mkutano Mkuu wa 13 wa KAUKI, Kidamali - Iringa


Mahudhurio ya Mkutano Mkuu wa 13 wa KAUKI hayakuwa ya Kuridhisha kutokana na baadhi ya Kanda kutokuwa na Uwakilishi. Kanda ya Kidamali, Magubike, Dar eS Salaam, Mafinga, Morogoro, Iringa Mjini na Kalenga ndizo zilizokuwa na Uwakilishi katika Mkutano huo. Kanda za Nduli, Mgongo, Itagutwa, Igominyi na Vilalo hawakuhudhuria Mkutano kwa sababu ambazo hazikuweza kufahamika.

Mojawapo ya mambo makubwa yaliyofanyika katika Mkutano huo ni pamoja na kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa Viongozi wa KAUKI watakaotumikia nafasi zao kwa kipindi cha miaka 3 kwa mujibu wa Katiba ya KAUKI.

Hali kadhalika Mada mbalimbali ziliwasilishwa kwa Wanaukoo zikiwa na lengo la kuwajengea uwezo na pia kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazowakabili wanaukoo.

Mkutano wa KAUKI wa 13 pia ulijadili changamoto mbalimbali zinazoukabili ukoo wa Kivenule na namna ya kuweza kuzitatua. Changamoto hizo ni pamoja na migogoro ya ardhi baina ya Ukoo wa Kivenule na Mwekezaji, ambao ulichukua sehemu kubwa ya ardhi. Mgogoro ardhi unaligusa eneo la Ulefi na eneo la Magubike, ambapo haya maeneo yaliyotwaliwa na Mwekezaji yalikuwa chini ya Umiliki wa Ukoo wa Kivenule na hata ushahidi wa Makaburi ya Waasisi wa Ukoo yapo kwenye hiyo ardhi iliyotwaliwa.

Mzee Bernard Hussein Kivenule akiwa na Dada zake wakati wa Mkutano Mkuu wa 13 wa KAUKI - Kidamali Iringa.

Changamoto nyingine kuzorota kwa mahusiano baina ya Wanaukoo na kutofanyika kwa Mikutano ya KAUKI toka mwaka 2017.

Pia Mkutano huo ulikuja na mpango madhubuti wa ukusanyaji wa michango na pia kuendelea kuboresha Mikutano Mikuu ya Ukoo ya Kivenule.

Wanaukoo wote kwa pamoja walikubaliana kwamba wataanza kutumia M-Koba kama njia madhubuti ya Ukusanyaji na Utunzaji wa Fedha za Michango toka kwa Wanaukoo.


Usiku wa Chakula Maalum kwa Wanaukoo - kilichofanyika wakati wa Mkutano Mkuu wa 13 wa KAUKI

Jumla ya Ahadi ya Shilingi Milioni 1,250,000 zilipatikana kwa ajili ya Mkutano Mkuu wa 14 wa KAUKI, utakaofanyika Kijijini Kidamali. Aidha kiasi cha shilingi 130,000/-  taslimu zilipatikana wakati wa Mkutano huo ikiwa ni michango iliyotokana na ahadi toka kwa Wanaukoo kwa ajili ya Mkutano Mkuu Ujao wa KAUKI.

MABORESHO KATIKA MKUTANO MKUU WA 13 WA KAUKI

Moja ya eneo lililoboreka kwenye Mkutano Mkuu wa Ukoo wa Kivenule ni kuongezeka kwa Bajeti ya Mkutano na pia Wanaukoo kuwa katika Mavazi rasmi ya Mkutano huo. Wanaukoo wa Kanda ya Dar es Salaam, Dodoma, Mafinga na Morogoro walijitoa kwa hali na Mali kwa lengo la kufanikisha Mkutano Mkuu wa 13 wa KAUKI. Hii ndiyo sababu ya kuboreka kwa bajeti ya Mkutano huo.

Mkutano wa 13 wa KAUKI uliandaa Usiku Maalum kwa Wanaukoo – Dinner Night Gala kwa Wanaukoo ambapo walijumuika pamoja, kunywa, kula na kubadilishana mawazo. Hili likuwa ni tukio adhimu ambalo lilikuwa halijawahi kutokea katika Mkutano wowote wa KAUKI.

Wanaukoo wakiwa katika Vazi la Tshirt Maalum zenye Nembo ya KAUKI waliupendezesha Mkutano Mkuu wa 13. Tshirt zenye rangi ya Kijivu, Nyeupe, Bluu na Rangi ya Damu ya Mzee zilivaliwa na Wanaukoo na Kuupamba Mkutano.

Imeandaliwa na:

 

Adam Alphonce Kivenule

Katibu Mkuu - KAUKI

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni